Ripoti kuu Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa Mwaka wa Fedha 2022/23

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,926
12,212
Ripoti ya mwaka ya ukaguzi wa Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa mujibu wa Ibara ya 143(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na Kifungu cha 34 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sura ya 418.

Ripoti hii inawasilisha matokeo ya ukaguzi na mapendekezo ya hatua za kuchukua ambazo zinalenga kukuza uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya rasilimali za umma.

MUHTASARI

Taarifa hii inachambua matokeo na mapendekezo yaliyopatikana kutokana na ukaguzi wa taarifa za fedha na uzingatiaji wa sheria katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, na Wakala za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023. Ukaguzi ulihusisha taasisi 475 zikiwemo mafungu 64, ofisi za Balozi 43, Wakala za Serikali 30, mifuko maalumu 19, vyama vya siasa 19, hospitali za rufaa na maalumu 34, na taasisi nyingine 266.

Bajeti

Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Serikali ilikusanya Sh. trilioni 41.880, zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa ya Sh. trilioni 41.480, ikiwa ni ongezeko la makusanyo kwa Sh. bilioni 400. Aidha, nilibaini ongezeko la makusanyo la Sh. trilioni 3.582, sawa na asilimia tisa ikilinganishwa na Sh. trilioni 38.298 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha uliopita wa 2021/22.

Makusanyo ya ndani yanayotokana na kodi, mapato yasiyotokana na kodi, na makusanyo ya Halmashauri yalifadhili bajeti kwa Sh. trilioni 26.515 (63%), wakati Sh. trilioni 15.365 (37%) zilitokana na misaada na mikopo (Sh. bilioni 759 za Misaada na Sh. trilioni 14.606 za Mikopo).

(ii) Hati za Ukaguzi
Kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, nimetoa hati za ukaguzi kwa taasisi 475 zilizowasilisha taarifa za fedha kwa ajili ya ukaguzi. Hati 471 zilikuwa zinaridhisha, moja ilikuwa hati yenye shaka, moja ilikuwa hati mbaya, na nilishindwa kutoa maoni kwa taasisi mbili. Aidha, nilifanya ukaguzi wa hesabu jumuifu za serikali ambapo nilitoa hati yenye shaka.

(iii) Utekelezaji wa Mapendekezo ya kaguzi za miaka ya nyuma pamoja na Maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023, kulikuwa na mapendekezo 7,342 ya ukaguzi yaliyotolewa miaka iliyopita. Tathmini yangu imebaini kuwa mapendekezo 2,946 (40.1%) yametekelezwa, mapendekezo 2,725 (37.1%) yalikua katika hatua mbalimbali za utekelezaji, mapendekezo 617 (8.4%) hayakutekelezwa, mapendekezo 366 (5%) yamepitwa na wakati, na mapendekezo 688 (9.4%) yamerudiwa kutokana na kuendelea kuonekana.

Vilevile, uhakiki wa utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ulionesha kuwa, kati ya maagizo 96 ya kamati kutoka katika ripoti zangu za miaka iliyopita, maagizo 38 (39.6%) yalitekelezwa kikamilifu, maagizo 43 (44.8%) yalikua katika hatua mbalimbali za utekelezaji, maagizo matano (5.2%) hayakutekelezwa, wakati agizo moja (1%) limerudiwa, na maagizo tisa (9.4%) yamepitwa na wakati.

Kodi, Mapato yasiyotokana na Kodi, Deni la Taifa na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali

Usimamizi wa Kodi

Tathmini ya utendaji na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya kodi katika mwaka wa fedha 2022/23, ilibaini kesi 967 za kodi kwenye Mahakama za Rufani zenye thamani ya Sh. trilioni 10.48, ikiwa ni ongezeko la Sh. trilioni 5.65 sawa na 117% ikilinganishwa na Sh. trilioni 4.83 za mwaka uliopita, ongezeko hili lilichangiwa na kuchelewa kwa uteuzi wa wajumbe muhimu wa kusikiliza kesi za rufani za kodi pamoja na ufinyu wa bajeti.

Pia ukaguzi ulibaini uwepo wa lita 1,105,466 za mafuta yaliyopitiliza muda wa kukaa nchini zaidi ya siku 30 za kisheria ambayo yalipaswa kwenda nchi jirani yenye ushuru wa forodha unaokadiriwa kuwa Sh. milioni 929.6 hivyo kuna hatari ya kutumika nchini bila malipo ya kodi.

Makusanyo yasiyotokana na Kodi
Ukaguzi ulibaini taasisi mbili za serikali kampuni ya ulinzi ya SUMA JKT na Jeshi la Uokoaji na Zimamoto (Fungu 14) hazikukusanya jumla ya Sh bilioni 1.86 baada ya kushindwa kutoa huduma, vituo vinne vya ukaguzi wa afya katika mipaka, bandari na viwanja vya ndege vilishindwa kukusanya tozo za ukaguzi Sh. milioni 879.11 baada ya ukaguzi na Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi (PHAB) haikukusanya kiasi cha Sh. milioni 768 kutoka kwenye vituo 2,640 vya Afya vilivyosajiliwa upya.

Nilibaini Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ulitoa mikopo ya Sh. bilioni 1.13 kwa vikundi vya wanawake na watu binafsi bila kuikatia bima. Pia, nilibaini kati ya mikopo hiyo iliyotolewa ya Sh. milioni 664.50 zimeshindwa kurejeshwa kwa muda wa miaka saba hadi 20, huku Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikishindwa kukusanya Sh. bilioni 32.43 zilizotolewa kwa Halmashauri ili kutekeleza mipango ya upimaji na umilikishwaji wa hati miliki za ardhi baada ya kumalizika kwa muda wa urejeshwaji wa fedha hizo tarehe 30 Juni 2022.

Katika Hospitali za rufaa, nilibaini kuwa Hospitali nne za rufaa zilishindwa kukusanya Sh. milioni 452 kwa kushindwa kufuatilia fedha za matibabu ya wagonjwa wanaotumia bima za mifuko mingine, wakati Sh. milioni 111.76 hazikukusanywa baada ya hospitali tatu za rufaa kutoa misamaha ya gharama za matibabu kwa wagonjwa wasio na sifa za kupata misamaha ya matibabu.

Aidha, nilibaini kuwa Sh. bilioni 61.09 hazikukusanywa na Taasisi 29 licha ya kutoa huduma, fedha hizo zimeripotiwa kama madai, nilibaini uwepo wa Sh bilioni 4.058 katika akaunti za taasisi tano za serikali zilizokaa muda mrefu bila kutumiwa na Sh. bilioni 7.73 zilikusanywa na taasisi tatu nje ya mifumo ya ukusanyaji.

Katika hali nyingine, nilibaini Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) iliingia makubaliano ya upangishaji eneo la ardhi lenye mita za mraba 11,000 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa shughuli za kibiashara kwa masharti nafuu yanayopelekea ukusanywaji mdogo wa mapato ya serikali, malipo ya pango kwa mita mraba yalikuwa dola za Marekani 4.36 tangu mwaka 1995 hadi mwaka 2018, ambayo yalipunguzwa hadi dola za Marekani 4.09 kwa mita mraba.

Usimamizi wa Deni la Serikali
Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023, deni la serikali lilikuwa Sh. trilioni 82.25 likijumuisha deni la ndani na nje Sh. trilioni 28.92 na Sh. trilioni 53.32 mtawalia ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na deni la mwaka 2021/22 la Sh. trillioni 71.31. Ongezeko hilo limesababishwa na mikopo halisi (Mapokezi ya mikopo mipya dhidi ya ulipaji wa mikopo).

Deni la Serikali ni himilivu, kwani uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Serikali (deni la nje na deni la ndani) kwa Pato la Taifa (GDP) umebaki kuwa chini ya kiwango ukomo/elekezi. Hata hivyo, nilibaini kuwa vihatarishi vya deni la nje bado vipo kiwango cha wastani kama ilivyokuwa mwaka uliopita. Hii ilichangiwa na uhafifu wa mauzo ya nje (exports).

Usimamizi wa Matumizi
Nimebaini kuwa taasisi saba zimekiuka kanuni za fedha kwa kuwa na bakaa ya fedha kiasi cha Sh. bilioni 2.45 katika akaunti zao za matumizi za masurufu. Pia, taasisi 13 zilifanya malipo ya Sh. bilioni 2.87 bila kudai stakabadhi za kielekitroniki kutoka kwa wauzaji wa bidhaa na watoa huduma.

Pia, ukarabati wa jengo la ofisi ya Balozi Kampala, Uganda haujaanza licha ya kuwa na bakaa ya fedha Sh. bilioni 1.78 tangu mwaka 2018. Kumekuwa na gharama kubwa za kodi ya pango ya kiasi cha Sh. bilioni 18.46 kwa majengo ya ofisi na makazi katika balozi 39 za Tanzania nje ya nchi kwa mwaka wa fedha 2022/23.

(vi) Usimamizi wa Ununuzi
Nilibaini, taasisi 25 hazikutekeleza mipango yake ya ununuzi yenye thamani ya Sh. bilioni 565.49, mamlaka nne za maji zilifanya ununuzi wa jumla ya Sh. milioni 537.93 bila kuwa na mipango ya ununuzi ya mwaka; na taasisi sita zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 1.82 bila kujumuishwa katika mipango yao ya ununuzi ya mwaka. Nilibaini miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 635.12 ilianza bila kuwa na cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira na kijamii, wakati ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 7.12 kwa taasisi 15 ulifanyika bila kuidhinishwa na bodi za zabuni.

Pia nilibaini upungufu kwenye michakato ya utoaji wa zabuni, ambapo taasisi 16 zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 149.56 bila kutumia mfumo wa kielekitroniki. Taasisi sita zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 77.67 bila kutumia njia za ushindani wa bei. Ununuzi wa bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni 2.16 ulifanyika bila kutumia mikataba na mikataba yenye thamani ya Sh. bilioni 4.78 haikupekuliwa na Wanasheria.

Aidha, nilibaini mapungufu katika kutimiza majukumu ya kimkataba ambapo taasisi 11 zilichelewa kulipa madai ya Sh. bilioni 38.73 na kutolipa madai ya Sh. bilioni 19.37 ndani ya muda uliokubaliwa. Wizara ya ujenzi haijalipa riba ya Sh. bilioni 17.48 Iliyotokana na uamuzi wa usuluhishi uliofikiwa tangu mwaka 2014, pamoja na riba ya Sh. bilioni 34.82 iliyotozwa kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuchelewa kulipa wakandarasi. Pia, mikataba 46 ya ujenzi ilikosa dhamana za utendaji kazi zenye thamani ya Sh. bilioni 383.76.

Nilibaini kuwa, Tume ya Madini na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) hazikudai dhamana ya utendaji kazi na malipo ya awali yenye thamani ya jumla Sh. milioni 675.90 kwenye mikataba iliyositishwa. Zaidi ya hayo, nilibaini miradi iliyotelekezwa yenye thamani ya Sh. bilioni 7.12 na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 200.01.

Ukarabati wa jengo la zamani la ubalozi wa Tanzania, lililoko kwenye Barabara ya 2139 R-Street, NW Washington, DC 20008, USA yalikuwa na dosari zifuatazo: gharama ya mkataba iliyonukuliwa ilizidi gharama iliyokadiriwa na mshauri elekezi kwa asilimia 94, ukarabati haukujumuishwa katika mpango wa ununuzi wa mwaka. Aidha, kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani cha asilimia 20 kilichotajwa katika mchanganuo wa gharama za kazi na ambacho kililipwa katika malipo ya awali hakikuwa na uhalisia kwa kuzingatia kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani ya Washington ambayo ni asilimia sita. Kulikuwa na hatari ya kulipa riba kwa mkandarasi kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya hati za madai (IPCs) Na. 1 na 2 ambazo zilitolewa tarehe 15 Machi 2023 na 05 Mei 2023, mtawalia, na hazijalipwa mpaka sasa. Mkandarasi alikuwa anawasiliana moja kwa moja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pasipo kumtumia Meneja Mradi.

Nilibaini kuwa Bohari Kuu ya Dawa ilinunua mashine 10 za kuondoa maumivu, ukakamavu na mkazo wa misuli (Diathermy) kwa bei ya Sh. milioni 136.7 na kuacha kununua vifaa hivi kwa mzabuni aliyebainika kuwa na bei ndogo wakati wa ushindani ya Sh. Milioni 103.2 hivyo kupelekea gharama za ziada ambazo zingeweza kuepukika za kiasi cha Sh. milioni 33.5. Vilevile nilibaini ununuzi wa vifaatiba kwa wazabuni 32 waliopewa zabuni zenye thamani ya Sh. bilioni 4.14 bila kufanyiwa uchambuzi wa awali na kuidhinishwa na bodi ya zabuni. Pia vifaatiba vyenye thamani ya Sh. bilioni 13.37 ambavyo ununuzi wake haukuwa umeanza.

Pia, nilibaini uchelewaji wa ununuzi na usambazaji wa vifaatiba katika vituo vya afya kwa siku zinazoanzia 23 hadi 1,458 tangu fedha zilipopokelewa na Bohari Kuu ya Dawa hadi vifaatiba vilipofika kwenye vituo vya afya, pia vituo 21 vya afya vilipokea vifaa vyenye thamani ya Sh. bilioni 1.68 ambavyo vilikuwa havijaanza kutumika.

(vii) Usimamizi wa Mali na Madeni
Ukaguzi wangu ulibaini uwepo wa mali 522 ambazo ni vifaa na magari, vilivyoachwa kwa muda mrefu bila kutumika. Nilibaini pia majengo chakavu na yaliyotelekezwa katika wizara, idara na wakala za serikali tano, ofisi za balozi tano, pamoja na uwepo wa viwanja ambavyo havijaendelezwa katika ofisi tatu za Balozi.

Katika ukaguzi wa Mfuko wa Mikopo kwa Watumishi wa Umma, nilibaini hasara ya Sh. bilioni 5.73 ambayo ilitokana na kutokurejeshwa kwa mikopo iliyotolewa kwa wafanyakazi kutokana na sababu mbalimbali kama vile vifo, kufukuzwa kazi, kujiuzulu, au kuachishwa kazi. Zaidi, mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 2.10 ilitolewa kwa wafanyakazi, lakini haijaanza kufanyiwa marejesho.

Katika Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, nilibaini hasara inayotarajiwa kutokana na uwepo wa mikopo chechefu yenye thamani ya Sh. bilioni 20.43, ambayo ni sawa na 80% ya mikopo yote ambayo bado haijalipwa hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023.

Kuhusu usimamizi wa madeni, nilibaini malimbikizo ya riba ya Sh. bilioni 103.22 kwa kushindwa kulipa madai ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) yanayohusiana na ujenzi wa Daraja la Nyerere (Kigamboni). Katika Ubalozi wa Tanzania New York, kodi ya majengo na riba ilifikia jumla ya dola za Marekani 847,888.40 (sawa na Sh. bilioni 2.16) kwa majengo mawili. Kodi hii na riba imetokana na kuondolewa kwa kinga ya kidiplomasia katika majengo hayo kutokana na uchakavu na kutokukarabatiwa kwa muda mrefu. Pia nilibaini kwamba, deni la Jeshi la Polisi la Tanzania linalodaiwa katika Dola za Marekani limeongezeka kwa Sh. bilioni 24.10 kutokana na kuchelewesha malipo. Ongezeko hili limetokana na mabadiliko katika viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni.

Pia, taasisi 97 ziliripoti jumla ya madeni ambayo hayajalipwa kwa zaidi ya miezi 12 yenye thamani ya Sh. trilioni 1.88, sambamba na kuwapo kwa madeni tarajiwa yenye thamani ya Sh. bilioni 626.89 kwenye taasisi 17 yanayosubiri uamuzi wa mahakama juu ya mashauri ya kisheria.

(viii) Ufanisi katika Utendaji

Usimamizi wa Fedha

Ukaguzi wangu ulibaini usimamizi usioridhisha wa fedha katika Wizara, Idara na Wakala za serikali. Nilibaini gharama za ziada katika miradi ya miundombinu ya barabara kiasi cha Sh. bilioni 13 zilizosababishwa na makosa ya awali katika usanifu na mapitio ya usanifu ambayo hayakuweza kuonesha mahitaji halisi yanayohitajika katika eneo la ujenzi. Pia, nilibaini kutolipwa kwa tozo ya ucheleweshaji wa ushushaji wa mafuta Sh. bilioni 18.94 kutokana na ufuatiliaji usioridhisha na kutokutekelezwa kwa makubaliano ya mkataba. Zaidi, nilibaini kutowasilishwa kwa dhamana ya fedha kutoka kwa makampuni ya madini yenye jumla ya Sh. bilioni 335.16, na hasara ya upotevu wa mapato ya kiasi cha Sh. bilioni 9.93 kutokana na maji yanayopotea.

Pia, nilibaini usimamizi wa fedha usioridhisha unaohusisha Hospitali Maalumu, Hospitali za Rufaa. Ikihushisha masuala muhimu kama upotevu wa mapato ya Sh. bilioni 8.94 kutokana na kukataliwa kwa madai ya huduma ya bima ya afya na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kutolipa kwa wakati madai ya Sh. bilioni 12.52 ya gharama za matibabu kwa hospitali maalumu na za rufaa. Aidha, Bohari Kuu ya Dawa kukaa na fedha za hospitali kiasi cha Sh. bilioni 10.13 kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kusambaza dawa, vifaatiba na vitendanishi, pia Hospitali za rufaa kuingia gharama za ziada za Sh. milioni 115.50 zilizotokana na ununuzi wa dawa na vifaatiba kutoka kwa wasambazaji binafsi, pamoja na vifaa vyenye thamani ya Sh. bilioni 3.47 vilivyo nunuliwa na Hospitali za Rufaa lakini havitumiki.

(b) Ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, na Miongozo
Nilibaini kutoteketezwa kwa dawa za thamani ya Sh. Bilioni 1.99 zilizokwisha muda wake wa matumizi, pia nilibaini mapungufu katika uendeshaji wa vitengo vya afya mipakani na katika viwanja vya ndege.

Masuala yanayohusu Vyama Vya Siasa
Nilibaini vyama vitano vya siasa; yaani, Chama cha Kijamii (CCK), National League for Democracy (NLD), NCCR Mageuzi, African Democratic Alliance (ADA) TADEA na Union for Multiparty Democracy (UMD), vilikusanya michango kutoka kwa wanachama mbalimbali jumla ya Sh. milioni 104.08 bila kuziwasilisha katika akaunti za benki za vyama husika. Hii ni kinyume na kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura ya 258 iliyorekebishwa mwaka 2019] kinachotaka kila chama cha siasa, ambacho kimesajiliwa kisheria kufungua akaunti ya benki ya chama, ambayo mapato yote yanayopatikana kuwasilishwa benki.

Kwa kuongezea, nilibaini kuwa vyama vinne vya siasa, yaani; Alliance for Africa Farmers Party (AAFP), Demokrasia Makini (DM), National Reconstruction Alliance (NRA), na National League for Democracy (NLD) havikuwasilisha tamko la kila mwaka la mali zinazomilikiwa na vyama hivyo kwa Msajili wa vyama vya siasa kwa mwaka ulioisha tarehe 30 Juni 2023.

(d) Usimamizi wa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji (CBWSO)
Nilibaini upungufu wa upatikanaji wa mtandao wa maji katika vyombo vya watoa huduma ya maji (CBWSO), hivyo kuathiri uendelevu wa miradi ya maji inayosimamiwa na vyombo vya watoa huduma ya maji hali inayochangiwa na ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi na kushindwa kukusanya mapato ya Sh. bilioni 1.64.

Pia soma: CAG Kichere: Licha ya kupewa Ruzuku ya Tsh. Bilioni 31.55, ATCL imepata hasara ya Tsh. Bilioni 56.64, ongezeko la 61% kutoka hasara ya Mwaka 2021/22
- Ripoti 21 za CAG zatua Bungeni kwa ajili ya kuanza kujadiliwa
 

Attachments

  • Ripoti_Kuu_ya_Ukaguzi_wa_Serikali_Kuu_kwa_Mwaka_wa_Fedha_2022_23 (1).pdf
    4.5 MB · Views: 7
Back
Top Bottom