Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud atembelea Taasisi ya JKCI, apongeza utendaji

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,854
12,090
Rais wa Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud amewapongeza wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma nzuri wanayoitoa ya kuokoa maisha ya watu wenye matatizo ya moyo.

Rais Hassan Sheikh Mohamud alizitoa pongezi hizo Aprili 27, 2024 Jijini Dar es Salaam alipotembelea Taasisi hiyo (JKCI) kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Akiwa katika Taasisi hiyo Rais Mahamud alitembelea maeneo mbalimbali ya JKCI ikiwa ni pamoja na mtambo wa Cathlab ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalumu kwaajili ya kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo.
Picha no. 1.jpg

Rais wa Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati alipotembelea taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Akizungumzia kuhusu ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI ni moja ya Taasisi inayoongoza katika nchi za Afrika Mashariki na kati katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Dkt. Kisenge alisema Rais Mohamud alitembelea Taasisi hiyo kwaajili ya kuona namna ambavyo nchi ya Somalia itawapeleka wagonjwa wa moyo JKCI kupata tiba ya matibabu ya moyo.

Picha no.5.jpg

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akimwelezea Rais wa Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud kuhusu huduma ya upasuaji mdogo wa moyo inayotolewa katika mtambo wa Cathlab wakati Rais huyo alipotembelea leo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Picha no.3 (1).jpg

Rais wa Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Picha no.4.jpg

Rais wa Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud akiangalia video fupi inayoonesha huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati alipotembelea Taasisi hiyo kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

“Nchi ya Somalia inawapeleka wagonjwa wengi wa moyo kwenda kutibiwa katika nchi za India, Ulaya na Marekani wakati huduma hii inapatikana nchini Tanzania, na ukiangalia nchi hizi ziko karibu hivyo basi itakuwa ni rahisi kwao kuwaleta wagonjwa kuja kutibiwa hapa kwetu”.



“Kuja kwa wagonjwa hawa kutaisaidia nchi yetu kukua kiuchumi kwani pesa zitakazopatikana zitawafikia watu wengi ikiwemo wamiliki wa hoteli ambako wagonjwa watalala pamoja na wafanyabiashara watakaowauzia vyakula na mahitaji mengine”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alimshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzidi kuimarisha mahusiano na nchi za nje ndiyo maana watu wengi wanakuja kuwekeza hapa nchi hata Taasisi hiyo imekuwa ikiwapokea wageni mbalimbali kutoka nchi za nje.

Akiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mhe. Rais Hassan Sheikh Mohamud pamoja na ujumbe wake aliambata na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu.
 
Back
Top Bottom