mwanamwana
JF-Expert Member
- Aug 1, 2011
- 1,077
- 4,114
Bertha Mabula amesema anahofia usalama wake kwa madai ya kubaini Polisi Mjini Kahama wanataka kumbambikia kesi ya ugaidi wakidai alitaka kulipua Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga wakati akifuatilia mwenendo wa shauri lake kwa ajili ya kukata rufani.
Bertha amedai alifika Mahakama Kuu kwa ajili ya kuchukua mwenendo wa shauri la madai dhidi ya mfanyabiashara Tumsime Tibaijuka ili akakate rufani kwa kutoridhishwa na uamuzi wa mahakama hiyo.
"Wakati naenda mahakamani Shinyanga nilikodi teksi inayoendeshwa na Beatus Mandali, alinifikisha akanisubiri nilipomaliza kupata huduma tuligeuza kurudi Kahama, nilipata taarifa kuna Polisi walikuwa wananisubiri maeneo ya Tinde wanikamate, lakini kwa bahati ilinyesha mvua kubwa, wakati tunapita eneo hilo hawakutuona.
"Siku ya pili nilipata taarifa dereva Beatus alikamatwa na askari akiwa katika kituo chake cha kazi, akapelekwa Kituo cha Polisi Kahama akituhumiwa kubeba gaidi anayetaka kulipua mahakama," amedai Bertha.
Amedai dereva alipofikishwa kituoni alihojiwa kisha akaachiwa na kuambiwa asimjulishe kuhusu tukio hilo, lakini dereva aliamua kumsimulia Bertha kuwa anatafutwa kwa tuhuma za ugaidi.
"Derava aliponiambia nilimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi kumfahamisha njama hizo na akaahidi atafuatilia tukio hilo.
"Niliendelea kuwasiliana naye kwa njia ya WhatsApp na meseji zote ninazo nikimfahamisha hofu yangu ya kubambikiwa kesi hiyo, akasema angekuja Kahama, lakini bado nasubiri huenda atakuja," amedai Bertha.
Dereva teksi, Beatus akithibitisha tukio la kukamatwa kwake kwa njia ya simu, amedai alikamatwa akiwa stendi anapofanyia kazi, askari walikwenda na karandinga la polisi kumkamata.
"Askari waliniambia wananikamata kwa sababu jana nilibeba magaidi walikuwa wamevaa hijabu, nilijibu niliyembeba kumpeleka Shinyanga mahakamani alikuwa kavaa dera.
"Walinikamata kwa kuwa nilikuwa na gari niliendesha gari yangu kuelekea Kituo cha Polisi Kahama huku nyuma nikisindikizwa na karandinga la Polisi.
"Nilihojiwa nikiwa katika ofisi ya upelelezi, niliulizwa jana nilienda wapi, nilijibu Shinyanga, nikaambiwa nilibeba magaidi wamevaa hijabu, nilijibu niliyembeba alikuwa kavaa dera, askari aliandika maelezo kwenye simu kubwa, mwingine alikuwa kabeba bunduki ndiye aliyekuwa ananipiga picha.
"Maelezo yalitumwa sikujua yalitumwa wapi, baada ya kumaliza mpelelezi, Edes Jackson aliniambia nisiende kumwambia mtu yeyote, lakini dada Bertha aliponipigia nilimwambia," amedai.
Amedai baada kumwambia Bertha alipigiwa simu na Afande Edes akamwambia alidhani ana bichwa kubwa anazo akili kumbe hana akili.
“Niliwindwa tangu mchana sikuwapo mjini, nilipoingia wakaja kunikamata, waliniambia walinivizia Tinde jana, lakini walishangaa nilipitaje hawakuniona.
"Nilikamatwa mbele ya watu wengi kituoni na waliponifuatilia kunitoa walijibiwa niko Polisi kwa ajili ya uchunguzi," amedai.
Askari mmoja anayetuhumiwa kuwapo katika msafara wa kumkamata dereva huyo alipopigiwa simu kuulizwa kuhusu tukio hilo, Afande Edes Jackson, alidai haruhusiwi kutoa taarifa yoyote kwa sababu sio msemaji.
"Unaniulizaje maswali hayo, sina mamlaka ya kutoa taarifa, muulize RPC Shinyanga, unakuja kwangu mwenye renki ndogo hivi, kwa akili ya utu uzima uliyonayo kwani mtu kukamatwa lazima aingizwe mahabusu.
"Unaweza kutuhumiwa ukakamatwa, ukapekuliwa na kuachiwa, hizo taarifa kaulize mkoani watakujibu alikamatwa, alikaa mahabusu muda gani msiniulize mimi," alidai Afande Edes akimjibu mwandishi kwenye simu.
Mfanyabiashara Tumsime anayetuhumiwa wakati dereva anakamatwa askari alimpigia simu kuuza shauri lilikuwa namba ngapi, alipoulizwa kwa kupigiwa simu kuhusu hoja hiyo alidai anamfahamu Bertha Mabula na walikuwa na kesi ambayo imeshatolewa uamuzi.
"Masuala kwamba nawafahamu askari waliomkamata dereva, mimi siwajui na kama alikamatwa kituoni kutakuwa na taarifa zake, huyo dereva wake pia simjui," amedai Tumsime.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Magomi amedai hana taarifa za Bertha kutaka kukamatwa kwa tuhuma za ugaidi.
"Taarifa za huyo mfanyabiashara kutaka kukamatwa mimi sina na bahati nzuri huwa nina tabia ya kukagua vitabu, Bertha Mabula, wala simjui.
"Kama anasema tuliwasiliana kwa simu labda nilisahau kama binadamu, sikumbuki, unajua kufanya kazi kwa simu mtu kama binadamu unaweza kusahau, mimi nipo aje kuniona," amedai RPC Magomi.
Baada ya shauri la madai kutupiliwa mbali, Bertha amewasilisha kusudio la kukata rufani akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Shinyanga kwa madai kwamba hakutendewa haki na ushahidi wake wa maandishi pamoja na mashahidi wengine watano wa upande wake haukuzingatiwa.
Pamoja na kufanya hivyo pia Machi 28, mwaka huu alimwandikia barua Jaji Kiongozi yenye kichwa cha habari kutoridhishwa na uamuzi uliotolewa na Jaji Frank Mahimbali, kwenye shauri namba 03/2023.
Katika shauri hilo, mdai Bertha Mabula dhidi ya Tumsime Tibaijuka na Tunel Incorporation Limited, anadai Sh. milioni 295 alizomkopesha Tumsime kwa ajili ya kufanya biashara, ambazo anadai hajawahi kuzilipa.
Chanzo: Nipashe