SoC02 Jamii mbili zinazochanganya

Stories of Change - 2022 Competition

Jade_

Senior Member
Apr 19, 2015
122
214
Hizi jamii mbili, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya jamii huchanganya sana watu. Inawezekana chanzo ni zote kuwa idara katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu. Au kwa sababu majina yote yana neno “jamii”. Hata maneno ustawi na maendeleo huonekana na walio wengi kama ni kitu kimoja.

“Si wote lengo lao moja bwana?!”

“Ndiyo hao hao! Kwani kozi wanazosoma chuoni si hizo hizo?!”

Kamusi ya Karne ya 21 iliyochapishwa na Longhorn Publishers 2011 inafafanua maendeleo kama ‘hali ya kupata ustawi’ . Neno ustawi kwenye muktadha huu lina maana ya ‘hali ya kukua vizuri au kufanikiwa; ufanisi, fanaka’.

“Sasa je? Mbona kama hizi jamii mbili zina maana ile ile?”

“Fasili zao zimebadilishwa maneno kidogo lakini ustawi na maendeleo ni kitu kimoja!”

Siku zote hivi vitu vidogo huleta tofauti kubwa.

Tuendelee kuchambua zaidi fafanuzi za haya maneno. Maendeleo kwa maneno mengine ni mwelekeo wa kupata ustawi au njia ya kuufikia huo ustawi. Ustawi ni lengo lenyewe kwa maana, neema tunayoitafuta tokea tuupate uhuru.


Untitled226-02.jpeg

Picha: Maendeleo ni njia ya kuufikia ustawi


Kama bado hujaelewa tofauti fikiria jambo hili. Kuna shida ya watoto yatima na waliopo kwenye mazingira hatari kuzagaa katika kata fulani. Tuangalie namna maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii zinavyofanya kazi kulingana na majukumu yao kutatua shida hii.

Idara ya Maendeleo ya jamii kupitia Afisa Maendeleo ya Jamii wa kata hiyo ana kazi ya kuhamasisha na kushirikiana na jamii kupata mawazo ili kuweza kutatua tatizo. Afisa huyu atasaidia kuitisha vikao kadhaa ndani ya kata, akishirikiana na viongozi wa mitaa, mtendaji wa kata, watendaji wa mitaa, pamoja na wananchi, ili waweze kakaa wajadiliane ni mbinu gani watatumia kutatua changamoto hiyo. Baada ya vikao, suluhisho la kujenga kituo cha kulea watoto yatima na waliopo katika mazingira magumu linapatikana. Wananchi wanajichanga, wanashirikisha nguvu zao kujenga majengo, wanaomba msaada serikalini na kwenye taasisi zisizo za kiserikali, na hatimaye wanafanikiwa kujenga kituo kwaajili ya hawa watoto.

Majukumu ya wanamaendeleo ya jamii yanatokana na historia ya nchi kama ilivyoelezwa katika Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996. Kiufupi sera hii inasema watu hawa wanawajibu wa kuiwezesha jamii kufikia malengo ya kimaendeleo ambayo yatapelekea ustawi wao kwa juhudi zao binafsi. Hii sera inaendeleza kusudi la Azimio la Arusha na dhana ya Ujamaa na Kujitegemea, kwamba, ustawi wa jamii hautaletwa na mtu mwingine ila jamii yenyewe. Jamii ni maendeleo na maendeleo hupelekea kutoweka kwa maadui wakuu, aliyowaainisha Hayati Julius Nyerere ambao ni umasikini, ujinga na maradhi.

Turudi katani kwetu ambapo kituo kimeshajengwa. Je hicho kituo wanakisimamia akina nani? Kituo hicho kinasimamiwa na mara nyingine kuendeshwa na ustawi wa jamii. Ustawi wa Jamii ni idara yenye jukumu la kutoa huduma mbalimbali kwenye jamii hasa kwa watu wenye mahitaji maalumu, pamoja na waliokosa wakuwawajibikia kama walemavu, watoto, wanawake nakadhalika. Huduma nyingine wanazotoa ni usuluhishi wa ndoa zenye mifarakano, huduma kwa watoto watukutu, matunzo kwa watu wenye ulemavu/wasiojiweza na majukumu mengine mengi. Huduma hizi mahususi zikifanyika kwa ufasaha basi jamii zetu zitakuwa zimeondokana na udhia mkubwa. Bahati mbaya mambo yanakuwa ndivyo sivyo.

Ndivyo sivyo inaanzia Wizarani wanapotoa maelekezo ya shughuli, hadi halmashauri za majiji, miji na wilaya. Kazi hazijulikani kama ni za maendeleo ya jamii au ustawi wa jamii. Viongozi na watu wa hizi idara mara nyingine hawaelewi majukumu yao ni yapi. Likija suala la pesa ndiyo kabisa utaona kila idara inavutia upande wake ili wasipitwe na fungu la baraka. Kuingiliana majukumu kuna sababisha mkanganyiko, ugomvi na uhasama. Hizi idara mbili zinaangaliana vibaya kana kwamba wale wa idara ya maendeleo ya jamii, au wale wa idara ya ustawi wa jamii wanaingilia majukumu yetu, au wanataka kazi zote zenye pesa wafanye wao.


Untitled226_20220802220604-01.jpeg

Picha: Migogoro kati ya Idara za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii


Mbaya zaidi, kushindwa kutofautisha na kuheshimu majukumu kuna punguza ufanisi katika kazi, na wanaoumia ni wananchi wa kawaida kabisa. Sehemu nyingi za nchi maafisa maendeleo wanafanya kazi za ustawi wa jamii na maafisa ustawi wanafanya kazi za maendeleo ya jamii pamoja na majukumu yao ya kawaida. Kata nyingi sana Tanzania hazina afisa maendeleo na afisa ustawi. Anakuwepo afisa mmoja kati ya hao na anafanya kazi zote mbili. Mbali ya kwamba mtu mmoja kufanya kazi za watu wawili ni kubeba mzigo mzito kuliko uwezo wa kimo, huduma za kijamii zinadorora pia.

Nini kifanyike? Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inabidi itilie mkazo majukumu yaliyokabidhiwa kwa sekta mbalimbali ndani ya wizara hiyo. Viongozi huko wizarani waelewe siyo tu wizara ilipo, bali ilipotoka na inapokwenda. Wa huko juu wakijipanga, wa huku chini watapangika. Migogoro ya kazi itapungua na kazi zitafanyika.

Ajira za watu waliosomea fani za ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii zitolewe kwa wahitimu ili waende kuziba mapengo yaliyopo kwenye kata kwa kukosekana kwa rasilimali watu wa kuhudumia jamii. Kila kata iwe na afisa maendeleo na afisa ustawi. Tuache kasumba ya kwamba mmoja akiwepo basi hakuna haja ya mwingine kuwepo. Wote wawili wanahitajika. Ikiwezekana hawa maafisa wawe na wasaidizi, sababu kuna kata hapa nchini zina eneo kubwa sana.

Hivyo basi, idara zote mbili ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu. Watu wa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii wanageuka sehemu ya jamii. Wanafanya kazi palipo jamii na jamii ndipo taifa linapoanzia. Jamii ikitetereka na taifa linatetereka. Kuweza kufahamu na kuainisha majukumu ya hizi sekta mbili tofauti, kutaweza kuhakikisha majukumu yao yanatekelezwa jinsi inavyopaswa. Itapelekea kuweza kujinasua kutoka katika matatizo yetu makuu, ambayo ni ujinga, maradhi, na umasikini, ili kila Mtanzania aishi maisha bora.
 
Karibuni kwa tafakuri, maswali au maoni kuhusu wizara nyeti ya maendeleo ya jamii.
 
Inawezekana matatizo mbalimbali yanayotokea ndani ya jamii yetu kama matatizo ya akili au watoto wa mitaani yangepungua kama idara za wizara ya maendeleo ya jamii zingepewa nafasi ya kufanya kazi zao kwa ufasaha.
 
Pia maelekezo ya kazi za maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii hutoka kwenye wizara mbili tofauti; Maendeleo ya Jamii na Tamisemi hivyo kuzidisha mkanganyiko.
 
Naendelea kutafakari juu ya hili swala la maendeleo ya Jamii. Kwanini jukumu la kufuatilia mirejesho ya mikopo inayotolewa na halmashauri wasipewe kitengo kingine hasa wanaohusika na mambo ya fedha? Shida ni watu wa maendeleo ya Jamii wanakuwa kama maafisa mikopo na muda mwingi hawafanyi kazi nyingine.
 
Naendelea kutafakari juu ya hili swala la maendeleo ya Jamii. Kwanini jukumu la kufuatilia mirejesho ya mikopo inayotolewa na halmashauri wasipewe kitengo kingine hasa wanaohusika na mambo ya fedha? Shida ni watu wa maendeleo ya Jamii wanakuwa kama maafisa mikopo na muda mwingi hawafanyi kazi nyingine.
Naona ni bora kianzishwe kitengo maalumu cha kufuatilia urejeshwaji wa mikopo ya halmashauri inayotolewa kwa vikundi mbalimbali. Kitengo hichi kiwe na msaada wa wanasheria pamoja na vyombo vya usalama kama polisi.
Watu wa maendeleo ya jamii bado watashiriki katika kuhakiki vikundi na kutambua waombaji na shughuli wanazofanya.
 
Napenda kuwakumbusha viongozi wa wizara ya maendeleo ya jamii kwamba wasome vizuri majukumu ya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii. Wasikae upande mmoja hizi idara ni mbili tofauti. Nasisitiza majukumu yao ni tofauti isije ikatokea kazi za idara mojawapo hazitekelezwi.
 
Back
Top Bottom