Maoni yangu: Je, wasanii wanapaswa kulaumiwa kwa mmomonyoko wa maadili hapa nchini?

Stephen Ngalya Chelu

JF-Expert Member
Oct 31, 2017
7,628
16,416
Na Stephen Chelu

Habarini waku,

Natumaini mko salama na mnaendelea na majukumu ya kuelekea uchumi wa kati na bila kusahau kujaribu kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Mungu atubariki kwa hilo, Amen.

Mimi sio mwandishi mzuri, kwa hiyo mnisamehe kama andiko hili litakuwa limekaa hovyo hovyo.

Basi pasi na kupoteza nielekee moja kwa moja kwenye mada, pia niseme tu kuwa huenda andiko hili linaweza kuwa refu kidogo lakini sidhani kama litakuwa refu kiasi cha kushindwa kosomeka kabisa. Leo nataka kujikita katika kujaribu kuangalia au kutoa maoni yangu juu ya lawama ambazo watu wa sanaa wamekuwa wakipewa kwa kudaiwa kuwa wanasababisha ama kuchangia kwa kiasi kikubwa cha mmong’onyoko wa maadili yetu ya kitanzania (ama kiafrika).

Nilipanga kufanya hivi siku za baadaye kidogo lakini nimejikuta naandika sasa kutokana na wimbi kubwa la kufungiwa kazi nyingi za sanaa (hasahasa zihusianazo na muziki) kwa sababu ya kudaiwa kuwa ziko kinyume na utamaduni na maadili yetu kama watanzania.

Tukianza kwa kujaribu kueleza maana ya maneno ‘utamaduni’ na ‘maadili’ katika mtizamo wa kijamii japo kwa ufupi. Maadili ni utaratibu wa kijamii ambao huwa na viwango juu ya usahihi wa matendo ya mtu katika jamii husika na utamaduni ni mjumuiko wa mawazo, mila na tabia za kijamii zinazopatikana katika jamii Fulani. Jamii ya bidanadamu inabeba makundi mengi sana ya watu wenye utamaduni na viwango vya kimaadili vinavyotofautina na makundi mengine. Kimsingi, utamaduni na maadili huweza kubadilika kadiri ya mabadiliko ya kiuchumi, mazingira au muingiliano kutoka katika jamii nyingine.

Nirudi kwenye lengo la andiko langu sasa,
Katika miaka ya karibuni jamii yetu imeshuhudia mabadiliko makubwa yana na kitamaduni na mmong’onyoko wa maadili yetu. Sisi sote ni mashahidi wa hilo. Na kati ya watu wanaowanaolaumiwa kwa hili ni baadhi ya wasanii wa muziki na filamu kwa kuchochea hili. Na katika katika kujaribu kukabiliana na tatizo hili, vyombo vyenye mamlaka ya kusimamia sanaa vimekuwa vikifungia baadhi ya kazi za sanaa ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa zikibeba maudhui yasiyofaa kulingana na jamii yetu ya kitanzania. Na katika kuendana na jitihada hizo, baadhi ya wanajamii nao wamekuwa wakiunga mkono na kupongeza hatua zinazochukuliwa na vyombo hivyo lakini pia kuna ambao pia huwa kinyume na maamuzi ya vyombo hivi pia.

Binafsi, suala la mmong’onyoko wa kimaadili kwa jamii yetu haliwezi kutizamwa na kushughulikiwa kirahisi kiasi hicho. Si sahihi mtu kusimama mbele ya watu na kusema “bwana, sisi miaka ya nyuma tulikuwa tunafuata misingi ya maadili haswa. Lakini tangu vijana wa siku hizi waingie katika kazi hizi za sanaa wameharibu kila kitu. Watoto wetu wameanza kuwaiga wao, na hawa wasanii wanakuja kutuletea kizazi cha hovyo kabisa” hapana, siyo kirahisi namna hiyo.

Tuna utaratibu utumikao dunia nzima katika kupata suluhisho la matatizo na kutatua changamoto mbalimbali. ‘utafiti’. Katika utafiti, ili tuje na hoja ya kwamba kitu Fulani kiko namna Fulani si lazima tuchunguze jumla ya vitu vyote vinavyohusika na lengo la utafiti, bali huchukuliwa sampuli kutoka kundi hilo na majibu yatakayopatikana katika sampuli hiyo ndiyo yatatupa hali halisi katika ujumla wa hicho tulichokuwa tunataka kukifahamu. Kwa hiyo, tukitaka kujua tabia ya kundi Fulani hatuhitaji kufanya utafiti kwa kila mtu apatikanaye katika kundi hilo ili tuthibitishe madai yetu, bali tutachukua baadhi kutoka kundi hilo na tutakachokipata hapo ndicho kitakachokuwa kipo katika kundi hilo zima. Pia kuna msemo wa kiingereza usemao ‘show me your friends are and I’ll tell you who you are’, (‘nionyeshe rafiki zako nami nitakuambia wewe ni nani’-Tafsiri ni yangu, siyo rasmi). Kwa kupitia vifani hivyo, tutaweza kuona kuwa matendo ya mtu mmoja mmoja yanategemea zaidi na kundi la kijamii ambalo mtu huyo hupatikana. Japo kuna haiba za kitofauti kati ya mtu na mtu, lakini asilimia kubwa ya utendaji wa binadamu huadhiriwa sana na kundi la ijamii linalomzunguka hivyo ni mara chache sana hutenda tofauti na jinsi ilivyozoeleka katika kundi husika.

Wasanii ni zao la jamii, wasanii ni wanajamii. Hakuna mwanasanaa yeyote hapa nchini kwetu ambaye amethibika kutoka anga au sayari za mbali kabisa huko. Wote hawa, tumekua nao, tuaishi nao na tunashirikiana sana tu katika mabo yetu mengi tu kama wanajamii. Na ndiyo maana upo msemo usemao ‘msanii ni kioo cha jamii’ kwa maana ya kwamba msanii hubeba na hutenda mambo yanayopatikana katika jamii yake. Ni sawa sawa na tunapojiangalia kwenye vioo vyetu majumbani kila siku, unapojiona kwenye kioo ndivyo hivyo wewe ulivyo. Ukiona jichoni kuna tongotongo, basi jua kuwa kioo hakijakudanganya, ni kweli una tongotongo. Sasa sindani kama mtu atakuwa na utimamu wa akili pale ambapo atakilaumu kioo kwa kumyonyesha kuwa yeye ana tongotongo, ndugu yangu, kioo hakidanganyi.

Wasanii ni vioo vya jamii, wayafanyayo yanaakisi uhalisia wa jamii yetu. Kwa sababu, msanii anapoimba nyimbo zenye lugha za matusimatusi anajua kuwa kuna watu wataupenda na kuushabikia. Msanii anapovaa nguo ki uchiuchi anajua ana uhakika kuwa kuna watu wataompongeza na kumuombna afanye zaidi na zaidi. Msanii hawezi kutumia gharama kuandaa kazi kwa gharama ili aandae kazi anayojua fika haitakuwa na wateja, hayupo. Kwa hiyo ukiona mtu anaimba matusi basi jua katika jamii kuna watu wanaopenda hivyo. Ukiona mtu anacheza uchi basi jua katika jamii kuna watu wanaopenda hayo. Kwa hiyo kusema kuwa wasanii wanaharibu maadili yetu si sahihi hata kidogo.

Kwani, wale wanawake wanaopita mabarabarani wakiwa wamevaa magauni ya kufanana wakicheza kwa kutikisa makalio hadharani watoto wakiwaangalia si ndiyo hao hao wakitoka hapo wanarudi majumbani kuwapikia chakula familia zao. Si ndo hao hao marafiki zetu. Wasanii wanaonekana kupenda ngono kwa sababu kwenye jamii yetu wapenda ngono tupo. Wasanii wanaimba nyimbo za matusi kwa sababu katika jamii watukanaji tupo tele, nakadhali nakadhalika.

Kwa hiyo kimsingi jamii haina mamlaka ya kuwalaumu wasanii, inatakiwa ijilaumu yenyewe. Jamii inawakataa wasanii wanaojaribu kwenda kinyume na mitazamo yao. Ukiangalia orodha ya juu ya wasanii wanaofanya vizuri kwa sasa wengi wao wanafanya kile ambacho watu wanasema si sahihi kulingana na utamaduni wetu, lakini mbona bado wako juu na wanakubalia? Ni kwa sababu wanakubalika na kundi kubwa zaidi la jamii yao. Kwa hiyo naweza kusema kuwa, wayafanyayo wasanii si chanzo bali ni matokeo.

KAMA WAO NI MATOKEO, CHANZO NI NINI HASA?

Kati ya karne ambayo huenda dunia imeshuhudia mabadiliko makubwa sana katika Nyanja mbalimbali za kimaisha basi ni karne ya 20. Lakini kilichotokea katika karne ya ishirini ni matokeo ya jitihada za kutoka karne za nyuma ambapo binadamu walikuwa wakijaribu kupambana na changamoto mbalimbali za kimaisha na kujikuta wakipitia hatua mbalimbali za kimabadiliko. Kabla ya karne ya ishirini dunia imeshuhudia muingiliano wa kijamii kutoka watu wa mabara tofauti, dunia ikashuhudua pia jitihada kubwa tu za kunyanyua technolojia na mambo mengine mengi. Lakini katika kupitia mabadiliko haya si jamii zote zilkuwa katika uwiano sawa. Kuna jamii zilizokuwa zimeendelea zaidi (ulaya na amerika) na jamii zilizokuwa nyuma (afrika,asia). Na matokeo yake yakawa ni kuwa jamii zenye nguvu zikazitawala jamii dhaifu na jamii dhaifu zikajikuta zinalazimika kubeba tamaduni za wenye nguvu.

Afrika tumesomwa na kimbunga cha utandawazi ilhali sisi tulikuwa bado hatujajiandaa kufika hapa. Tunaishi maisha ya watu wengine ambayo kimsingi sisi hatustahili kuwapo hapa kwa sasa. tusiwalauma wasanii. Sasa hivi tunaishi katika dunia unayoweza kupata au kuona chochote upendacho, ni wewe tu maamuzi yako. Na wasanii ndiwo kielelezo sahihi kabisa cha hapa tulipo lakini wao hawahusiki kwa namna yoyote kwa sisi kuwapo hapa.

SASA KAMA HAWAHUSIKI, NINI KINAFANYA WAHUSISHWE?

Wasanii wanalalamikiwa kwa huwa tu wao wanafuatiliwa na wanaonekana kirahisi kuliko watu wengine. Msanii Fulani akiwa na akibadilisha wanawake wane ndani ya miezi mitatu tutambebesha majina ya hovyo hovyo huku tukisahau sisi tuko kama yeye na hata zaidi yake ila kwa kuwa sisi hakuna anayetufuatilia tunajiweka katika kundi la wanakondoo wa Mungu. Tunawalalamikia wao huku sisi tukiwa kama wao huku tukitarajia tatizo litatatukuka kwa misingi hiyo. Hapana, hatutoweza kamwe.

TUFANYEJE SASA?

Kama tulivyoweza kuona kuwa, chanzo cha kukengeuka kimaadili kama taifa kuna mizizi mirefu sana kutoka karne ya nyuma kabisa, kwa hiyo ili tatizo hili litatuke inabidi itumike nguvu na maarifa makubwa sana tena sana. Hatuwezi kutokomeza haya kwa utaratibu wa kukwepa majukumu kwamba ‘fulani ndiye kafanya, sisi hatuhusiki’ ilhal tunajua kuwa sisi ni wamoja wao, hatuwezi kufika kwa njia ya kuwabebesha akina Fulani mizigo ya madhambi huku sisi tukiwa wadhambi wakubwa kuliko wao, hatuwezi na hatutoweza. Inabidi tukubali kuwa tulisombwa na kimbunga ilhali hatujajiandaa na tumefika eneo lisilotuhusu bila kutarajia, na kisha sote kwa ujumla tukubaliane kutokukubaliana na hali tuliyonayo sasa na tuingie katika tafakuri nzito tuone tutatokeje hapa. Ni jambo gumu sana lakini litawezekana tu kama tutakuwa tumeamua. Lakini tukiendelea na utaratibu wa sasa nitakuwa nisawa na kuziba mto kwa viganja, maji yatapita katikati ya mikono na vidole vyetu na ndipo tutakapojisemea mioyoni mwetu “ya nini kuhangaika na mambo yasiyo na faida? Tujiondokee zetu tukale na kunywa maana si sisi pekeyetu tutakao sumbuliwa na hili”.

Tukijiangalia kwenye kioo twajiona tu uchi, tutafute nguo tujisitiri….tusivunje kioo kwa maana kufanya hivyo kutafanya tubaki uchi daima dumu”

Nakubali kukosolewa kwa nia njema


Chelu, Stephen N.


Pia unaweza kusoma maandiko yangu mengine haya hapa chini

Wazazi na jamii, tusiwanyang'anye watoto utoto wao - JamiiForums


Mawazo haribifu huja wakati ukiwa dhaifu kifikra, kaa chonjo. - JamiiForums
 
Mkuu mimi binafsi huku huwa nafuata umbea - nani kafanya nini, nani kazushiwa nini... ikawaje.... Makala yako hii nzuri peleka kule Hoja na Habari Mchanganyiko. Huku leta habari za watu za uongo au za ukweli lakini sizizo na tija na tupicha picha.
 
Back
Top Bottom