SoC03 Kukuza ujuzi wa masomo ya kijamii kutaongeza uwajibikaji

Stories of Change - 2023 Competition

Tonytz

Senior Member
Jul 18, 2022
159
1,142
Ujuzi wa masomo ya kijamii ni taaluma ambayo inajumuisha masomo mbalimbali yanayozingatia utafiti wa jamii ya binadamu, miundo ya kijamii, taasisi za kijamii tabia na mienendo katika jamii na mwingiliano katika jamii. Maudhui katika masomo haya ya kijamii huchotwa kutoka vyanzo vya masomo mbalimbali kama vile historia, jiografia, uraia, sosholojia, anthrolopolojia, uchumi na sayansi ya kisiasa. Malengo mahususi ya masomo hay ani kwanza kutaka kukuza uelewa wa jamii ya wanadamu na ulimwengu unaozunguka na pili ni kukuza raia wenye uwajibikaji. Masomo haya ya kijamii siyo tu kwamba humsaidia mwanafunzi darasani bali huipa jamii mitazamo mbalimbali kuhusu jamii, kusaidia kuchanganua na kufasiri masuala ya kijamii, matukio mbalimbali ya kihistoria, kiutamaduni na kutegemeana kimataifa.

Katika andiko hili nitajikita katika kujadili kwa ufupi mambo makuu matatu ambayo; kwanza umuhimu wa kukuza ujuzi wa masomo ya kijamii, pili njia zitakazowezesha kukuza ujuzi wa masomo ya kijamii na mwisho namna ujuzi wa masomo ya kijamii utakavyoongeza uwajibikaji katika jamii.

UMUHIMU WA KUKUZA UJUZI WA MASOMO YA KIJAMII.

Kwanza,
huwezesha kuwasaidia wanajamii kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye Maisha ambazo hukutana nazo kila siku. Pili, ni chachu ya mabadiliko ya mabadiliko katika jamii, kwani ujuzi wa masomo ya kijamii husaidia kutengeneza au kuzalisha viongozi bora na wenye uzalendo kwa mustakabali wa Taifa letu. Uongozi bora huleta tija katika usimamizi wa miradi ya maendleo. Tatu, hukuza maadili na mielekeo chanya miongoni mwa wanajamii na jamii kwa ujumla. Jamii inapokuwa na watu wenye maadili hujijenga sana kiuwajibikaji. Ni muhimu jamii iwe na maadili yatakayotetea haki za binadamu na mali zao. Nne, huimarisha usatawi wa pamoja, kwani masomo haya ya kijamii huzuia au hutafuta suluhu ya mambo magumu ambayo yanaweza kuikumba jamii. Tano, huwapa wanajamii ujuzi unaohitajika ili kushiriki kikamilifu katika michakato ya kiraia na kidemokrasia. Kwa mfano kushiriki katika michakato ya upigaji kura ili kuchagua viongozi wan chi, kutetea haki za binadamu, kupinga rushwa na kutii mamlaka.

KUKUZA UJUZI WA MASOMO YA KIJAMII.

Kukuza ujuzi wa masomo ya kijamii ni kunajumuisha mchanganyiko wa fikra makini, tafiti, uchunguzi na mawasiliano Madhubuti. Kuna njia nyingi sana za kukuza ujuzi wa masomo ya kijamii lakini hapa nitaelezea chache tu.

Kwanza, kuchambua na kutathmini ukweli na uhalisia wa vyanzo mbalimbali vya taarifa kabla ya kuviweka bayana kwa jamii. Miongoni mwa matukio yanayoonyesha kukosekana kwa ujuzi wa masomo ya kijamii kwa Watanzania wengi ni tabia za baadhi ya watu kuweka taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii ambazo huweza kuleta athari kubwa sana kwenye jamii yetu. Kwa mfano, kuwepo na taarifa za matukio ya uzushi , taarifa kuchafua watu binafsi na viongozi ni ishara tosha ya kukosekana kwa ujuzi wa masomo ya kijamii miongoni mwa wanajami, kwani watu hawazingatii misingi ya kimaisha katika jamii. Hivyo mtu anayechambua na kutathmini chanzo cha habari au taarifa huongeza ujuzi wake katika jamii na masomo ya kijamii.
IMG_20230703_195348_266.jpg


Picha: mtandaoni
Pili, kwa kusoma Makala mbalimbali na tafiti. Mara nyingi ujuzi wa masomo ya kijamii huongezwa na kujengwa kwa kusoma vitabu, magazeti, Makala na nyaraka mbalimbali zinazohusiana na masomo ya kijamii. Kwa kusoma na kutafiti kunajenga tabia ya kujifunza vitu vipya kwenye jamii na kuongeza uelewa wa matukio mbalimbali katika jamii.

Tatu, kwa njia ya kuandika na mawasiliano ya mdomo. Kwa uandishi wa insha, barua, ripoti na kumbukumbu mbalimbali za kijamii kunaongeza ujuzi wa masomo ya kijamii.

Nne, kwa kushiriki katika shughuli zinazokuza ufahamu na ushiriki wa raia. Kwa mfano, kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijamii, kujiunga vikundi mbalimbali vya kijamii na vyama.

UJUZI WA MASOMO YA KIJAMII NA UWAJIBIKAJI.

Kwanza, kwa kuelewa masuala mbalimbali ya kijamii kama vile umasikini, ukosefu wa haki na usawa, ubaguzi na matatizo ya kimazingira, watu hufahamu wajibu wao katika kuyashughulikia. Maarifa na juhudi zinazochukuliwa na watu katika kutatua changamoto hizo hupelekea kuzalishwa kwa vitendo au tabia vinavyolenga kuleta matokeo yenye kuleta maendeleo katika jamii.

Pili, kama nilivyotangulia kusema mwanzoni kuwa masomo ya kijamii hujuisha tafiti juu ya mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo utamaduni wa jamii, hali hiyo hukuza uelewa wa kitamaduni. Kutokana na watu kuwa na uelewa wa kitamaduni, huweza kuishi Maisha Maisha ya kiuwajibikaji kwa kuwatendea mema wengine, kuacha ubaguzi, kushirikiana katika kazi na kujenga amani ambayo kwa pamoja huchochea uwajibikaji wenye kuleta maendeleo kwenye jamii, kwani hali hii huleta usawa.

Tatu, kwa kuchambua na kutafiti masuala mbalimbali ya kimaadili, hukuza ujuzi wa kifikra, kuamua kwa usahihi kwa mustakabali wa nchi na watu wake. Kupitia mijadala mbalimbali inayohusu maadili makanisani, shuleni, misikitini, kwenye makongamano pamoja na vyombo vya habari na kurasa za mitandao ya kijamii, watu hupata ujuzi na changamoto za kimaadili na namna ya kukabiliana nayo. Ujuzi huu husaidia kuwajibika Zaidi katika kukabili changamoto za kimaadili na kutafuta suluhu zenye kuleta usawa katika jamii.

Nne, kwa kujifunza michakato ya kidemokrasia kupitia tafiti za masomo ya kijamii, husaidia kukuza ushirikishwaji katika Nyanja mbalimbali. Masomo ya kijamii huwafunza watu kuhusu demokrasia, haki za binadamu na wajibu wetu kwenye jamii. Katika kujua michakato hii ya kidemokrasia hukuza ujuzi wa watu juu ya masuala mbalimbali ya kiuwajibikaji. Kwa mfano, kwa sasa raia wengi nchini Tanzania hushiriki katika kupiga kura, ili kuchagua viongozi wao, kutetea haki za raia na kujiunga na mashirika mbalimbali yanayofanya kazi ya kuboresha jamii.

Tano, kupanua uhusiano wa kimataifa. Katika masomo haya watu hujifunza historia, uchumi, tamaduni na teknolojia ya nchi nyingine, hali hii hukuza ujuzi wa kimahusiano ambapo uhusiano wa kimataifa huwawezesha watu kuelewa wajibu wao wa kiraia, kukuza maendeleo endelevu, kusaidia haki za binadamu na kufanya kazi kwa ushirikiano.

Sita, kwa kuelewa miktadha mbalimbali ya vyanzo vya masomo ya kijamii, humwezesha mtu binafsi na jamii kwa ujumla kufanya maamuzi yenye kuchochea maendeleo na uwajibikaji wenye tija katika Taifa.

Kwa kuhitimisha, naweza kusema kuwa ni muhimu kwa serikali kuchukua hatua Madhubuti ili kuweza kuweka misingi na mikakati itakayomfanya mwanafunzi ayaelewe masomo ya kijamii kwa vitendo ili jamii iweze kuepukana na matatizo sugu ya kijamii ambayo siku hadi siku yanaongezeka kama vile ushoga, usagaji,rushwa, migoro ya mapenzi na ndoa, migogoro ya ardhi, uwekezaji na uhujumu uchumi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali na watu binafsi.
 
Habari. Naomba msaada wa marekebisho kwenye tittle ya hii story, pale kwenye neno "masoko" isomeke "masomo"
Tittle iwe: kukuza ujuzi wa masomo ya kijamii kutaongeza uwajibikaji.#moderators
 
Habari. Mhusika yoyote,tafadhari naomba msaada kurekebishiwa tittle ya thread yangu hii, kwenye neno "masoko" isomoke "masomo"
Tafadhari naomba msaada huo . Naomba sana moderators mnisaidie hapo.
 
Back
Top Bottom